0
Ni dhahiri Tanzania imefika hapa kutokana na jitihada, uzalendo na mapenzi waliyokuwa nao vijana wa zamani. Vijana hawa wa zamani akina Mwalimu Nyerere, Mzee Butiku, Mzee Kaduma, Mzee Kingunge, Mzee Sokoine na wengine wengi walihakikisha wanapigana kwa ajili ya taifa letu ili liweze kupata ukombozi dhidi ya mataifa dhalimu ya kibepari.
Hivyo basi, ni jukumu letu sote vijana wa leo kuweza kuendelea kulipigania taifa letu dhidi ya utumwa mpya wa fikra unaoratibiwa na mataifa ya kibepari. Mataifa haya ya kibepari yanataka kuendelea kufurahia ukoloni mambo-leo na utumwa wa kifikra walioupenyeza Tanzania ili waweze kuchota rasilimali zetu na kutuacha tukibaki omba omba na kuzidi kuwasujudu wao.
Nani mwenye jukumu la kulipigania taifa letu na kulikomboa dhidi ya mabepari hawa kama sio sisi vijana?
Kilichonisukuma kuandika makala hii ni baada ya kuwa naongea na vijana wenzangu wakati fulani katika soga za jioni na tukawa tunajadili ni kwa namna gani taifa letu linatutegemea vijana. Hapo wimbi kubwa la vijana likaanza kuniandama na kusema kwanini tulisaidie taifa hili kwani lenyewe limetusaidia nini mpaka sasa? Hapo nilipigwa na butwaa nikapata kigugumizi nisijue cha kusema kwa dakika moja hivi.
Nikawa najiuliza kwani baadhi ya vijana wa leo tumepatwa na nini? Na inakuwaje fahari ya taifa hili hatuioni? Ama kuna kitu kimeingia kwenye akili zetu?
Baada ya ule mjadala na vijana wenzangu nikagundua mambo mengi sana ambayo yameanza kutupotosha vijana wa leo na kushindwa kuona kama tunajukumu lolote kwa taifa hili. Hebu kabla ya kuanza kuyajadili yale niliyoyagundua hebu tuone kwa ufupi ni kwa namna gani ubepari umefanikiwa kutawala fikra zetu vijana kiasi cha kuichukia kwa dhati kabisa taifa letu na kuona hatustaili kulitumikia hata kwa chembe moja.
Tutambue ya kuwa, nia kubwa ya ubepari (capitalism) ni kuhakikisha ya kuwa inavunja misingi ya imara ya usoshalisti (socialism) kwa kuhakikisha njia kubwa za uzalishaji zinakuwa chini ya watu binafsi badala ya serikali. Na pia inabadili umoja na kuwa ubinafsi na mwisho unawaaminisha watu ya kuwa ili kuweza kupata maendeleo lazima tuache ukale na kwenda kwenye usasa kama ule wanaouhubiri.
Yote haya hufanywa na mabepari kwa nia moja tu, kuweza kupata rasilimali kwa urahisi bila kupata vikwanzo kwani wao huonekana kuwa bora zaidi kwa kusaidia nchi zetu masikini kwa kutuletea vijipesa kidogo kwa mkono wa kushoto zenye masharti mengi na kuchukua malighafi nyingi kwa jina la uwekezaji.
Kwa kuwa wizi na unyonyaji huu umekuwa ukiendelea kwa muda mrefu sasa, imefika mahali vijana tumeona ni sehemu ya maisha yetu na hivyo hatuna cha kufanya zaidi ya kuendelea kuukumbatia mfumo huu ilimradi mkono wako uende kinywani kila siku.
Kile ambacho niligundua kutokana na majadiliano na vijana wenzangu ambao hawakudhani kama wanajukumu la kuisaidia taifa hili ni kama ifuatavyo:
Ubepari umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuimarisha ubinafsi’ baina yetu vijanana kile ambacho tunakijali ni sisi kufanikiwa na sio mtu mwingine wa ziada. Leo hii kila kijana ukizungumza nae anajaribu kuona ni kwa namna gani anaweza kufanikiwa yeye mwenyewe na hapa ndipo unapoona matukio ya watu wengi kujilimbikizia mali na ufisadi. Hii ndio picha halisi ya kile ambacho ubepari unataka tufanye bila kujali tunapata pesa nyingi kwa mgongo wa nani.
Hebu jiulize kidogo, hawa vijana wa zamani wangeamua na wao kuwa wabinafsi kwa kiwango hichi tungekuta chochote kimebaki katika taifa hii leo? Leo hii kila kijana anasema mbuzi atakula urefu wa kamba yake, sasa kama ndo hivyo hili taifa litarudi mikononi mwa mabepari muda mfupi. Tufanye hima vijana tuanze kupigana kwa maslahi ya taifa zima na tuache ubinafsi uliopandikizwa na ubepari.
Kitu kingine nilichogundua, sasa vijana tulio wengi tuna ndoto ya Marekani (American Dream). Leo hii vijana walio wengi ukiwasikiliza wanatamani kwenda Marekani kwenye nchi ya asali na maziwa ambayo wanaamini ya kuwa huko watanufaika zaidi ya hapa Tanzania. Hapa ndipo naposhindwa kupata mantiki ya vijana hawa wenzetu, ina maana mtu uko radhi kwenda kwa watu uende ukawanufaishe wao na kuacha taifa lako likiangamia?
Leo vijana walio wengi wanahusudu maisha na elimu ya ughaibuni wakiwa na dhana ya kwamba maisha bora hupatikana huko kuliko Tanzania. Hapa ndo tuone vile ubepari ulivyotuathiri kifikra kiasi cha kuona vitu vyote bora na vizuri hupatikana kwenye mataifa yao na vya kwetu bado ni vya kishenzi. Hapa mara nyingi huwa najiuliza ina maana tunapoamua kukimbilia huko kwa mabepari huwa tunasahau ya kuwa hayo maisha mazuri tunayoyaona kuna watu waliyandaa na kama ndivyo hivyo kwanini na sisi tusiandae maisha bora hapa kwetu ili tufurahi na kujivunia taifa letu?
Hivi sasa nchi za Umoja wa Ulaya na hasa mshirika wao mkuu Uingereza ameazimia kujitoa katika umoja huo endapo nchi hizo wanachama hawataweka zuio la kupokea wageni kutoka nchi za Afrika na Asia.
Kwa upande mwingine, mgombea urais nchini Marekani Donal Trump nae katika sera zake anasema akichukua dola la Marekani atarejesha wahamiaji wote wa kutoka bara la Afrika kwao. Sasa hapa ndo tuone vile mabepari hawa wakitaka nchi yao ibaki kuwa yao na sisi wengine hatuhitajiki sasa kwanini tusianze kulijenga taifa letu na kuacha kuwa na ndoto za kupenda kwa wengine ili hali tukiacha kwetu kusiwe nawakupaendeleza. Hima sasa vijana tupambane kuendeleza na kurejesha mapenzi na uzalendo katika taifa letu.
Tanzania itakombolewa na vijana wabunifu na wasomi, leo hii inatia simanzi kuona vijana wengi hatupendi kusoma kabisa vitabu ama majarida ambayo yatatufungua akili na kutuletea changamoto. Hulka hii ya kusoma vitabu imepotezwa na kile walichofanikiwa kukipandikiza mabepari mitandao ya jamii’. Hapa ndipo fikra zetu vijana zilipo kila mtu amezingatia kwa makini kuona yale wafanyao mabepari hao na kuendelea kufanya mambo yasio na manufaa kwa taifa letu zaidi ya kuendelea kuwa maskini.
Capitalism or Socialism
Tukitizama ubunifu kwa nchi yetu ni mdogo sana kwani vijana wengi hatuko tayari kufanya kitu kwa taifa letu. Kama hulka ya kujisomea vitabu na machapisho sambamba na mijadala yenye kuibua fikra makini na mbadala mbalimbali imekufa ni dhahiri ubunifu hautakuwepo kwani wengi wetu tunadhani baada ya kupata elimu ya chuo kikuu inatosha na hakuna zaidi ya kutafuta ajira. Hapa tukipata mkopo tukanunua gari na kujenga kanyumba basi tunaona tumemaliza kazi yote inabaki kula nchi tu.
Leo hii vijana wa nchi za kibepari wanakuja na ubunifu mbalimbali kila kukicha sisi tunabaki kuwa walaji wa ubunifu wao na kuzidi kuwatajirisha kwani tunaendelea kuwa waumini wazuri wa ubunifu huo. Hebu tizama kijana mdogo wa umri wa miaka 31 ndugu Mark Elliot Zuckerberg ndiye aliyegundua mtandao wa kijamiiFacebook na mpaka sasa umeweza kumpatia utajiri wa dola za Kimarekani bilioni 46. Hii inaonyesha vijana wa mataifa ya kibepari wanavyozidi kunufaika na mitandao hii ya kijamii ili hali inatuacha siye wa bara la Afrika tukizidi kuwatajirisha na sisi tukibaki kuwa ‘mazuzu’.
Kitu kingine kikubwa zaidi kinachotuathiri vijana wa leo ni uvivu (ndio uvivu). Wengi wetu wa vijana leo hii tunapenda starehe kuliko kazi vijana wa mjini leo huita ‘kula bata’.  Hapa sitaki kusema kuwa starehe ni mbaya na watu wasipate wasaa wa kustarehe la hasha! Ila, cha kuzingatia lazima tuwe na nidhamu na starehe tunazofanya kwani usipokuwa na nidhamu ndipo hapo tunaposhuhudia starehe zikiendelea kuwafanya maskini vijana walio wengi leo Tanzania.
Ukiangalia kwa umakini utakuta vijana wengi wanafanya starehe kila siku aidha baada ya kazi ama hata wakati wa kazi. Sasa ukijiuliza mtu anayefanya starehe kila kukicha je huwa anapata wasaa wa kufikiria kwa ajili ya hili taifa muda gani? Au vijana tunachojali ni sisi kufanya yanayotuhusu na wengine wajijua wenyewe na maisha yao.
Hii kasumba ya uvivu ndo inapelekea taifa letu kuendelea kudumaa na kushindwa kupiga hatua za maendelea, leo hii tunaona Rais Magufuli akiweka msisitizo katika ofisi za serikali watu kufanya kazi kwa kujituma kwa kuzingatia ueledi na kuacha uvivu. Taifa letu lilishazama katika dimwi hili na mtego huu wa kibepari kwani hapa mataifa ya Magharibi hufurahi kuona taifa vivu kwani hujua hapo ndipo wataweza kupata masoko ya kutosha na kuzidisha utegemezi kwao.
Fahari yetu leo kama vijana iko wapi na kama tunashindwa kujivunia nchi yetu sasa tumebakisha nini tujivunie kama watanzania?
Ni wakati sasa vijana wa Tanzania tukaamka na kuanza kubadilika kifikra ili tuwe huru na kuweza kufanya mambo yatakayomkomboa mama Tanzania kutoka kwenye manyanyaso, udhalimu na wizi unaofanywa na mataifa ya kibepari.
Ili taifa letu liweze kupiga hatua hatuna budi sisi vijana tuweze kulipigania kwa nguvu na dhamira halisi ndo tutaweza kuona taifa hili limetufanyia nini. Hii dhana ya kibepari tuliyonayo ya kutaka kupokea tu bila kutoa italifanya taifa letu lizidi kudumaa tukisubiri mabepari waje kutoa misaada ili kuendeleza kilimo chetu, viwanda vyetu, michezo yetu, elimu yetu na miundo mbinu yetu. Haya yote yanaweza kufanywa na vijana sie kwa kuonyesha ubunifu wa dhati na kulifanya taifa letu liweze kupiga hatua.
Mwalimu Nyerere anatukumbusha ya kuwa “Wale wanaopata hii fursa, hawana budi kuwalipa wengine walio jinyima kwa ajili yao. Ni kama watu waliopewa chakula kilichobaki wakati wa njaa katika kijiji ili waweze kupata nguvu kwenda kutafuta chakula kingine sehemu ya mbali.watu hao wakichukua chakula hicho na wasirudi na msaada kwa ndugu na jamaa zao basi wao watakuwa wasaliti. Vivyo hivyo, kama vijana watapata fursa ya kupata elimu ya watu wa nchi hii halafu wakawa na tabia za ukuu au wakashindwa kutumia elimu yao kuendeleza taifa hili watakuwa wasaliti wa muungano huu”.  

Post a Comment

 
Top