WATU wengi hutumia muda wao baada ya kazi kukaa na marafiki, makundi rika na wengine hufanya mambo ambayo huwazuia kuzifikia ndoto zao.
Wengine hutumia muda wao baada ya kazi kuongeza vipato vyao kwa kufanya miradi binafsi, kuongeza maarifa kwa kujisomea vitabu na majarida mbalimbali, kuhudhuria semina, mafunzo na makongamano.
Muda unaoutumia baada ya kazi unaweza kukuongezea mafanikio au kukupunguzia mafanikio yako katika maisha.
Siyo siri kwamba, muda unaotumia baada ya kazi unaweza ukakuongezea maisha au kukupunguzia maisha kulingana na yale unayoyafanya au hata na vile ulivyojipanga mwenyewe.
Simaanishi ufanye kazi kwa saa 24, la hasha! Hapa nazungumzia zile saa zinazosalia baada ya kazi ambazo watu huzitumia kujiachia, kujistarehesha, kujipumzisha baada ya kazi jambo ambalo ni zuri, siyo vibaya.
Muda huo watu wengine huutumia kufanya maongezi ambayo ni hasi, maongezi ambayo mara nyingi huyaharibu mafanikio yao na kuwazuia kuingia kwenye mafanikio wanayoyatamani.
Baada ya kazi kuna vitu vingi ambavyo unaweza kuvifanya unavyovipenda kama vile kujifunza ala za muziki, kujisomea kuongeza maarifa maana bila maarifa watu huangamia. Hata kwenye vitabu vitakatifu imeandikwa: “Watu wangu huangamia kwa kukosa maarifa”.
Tunapaswa kujijengea tabia ya kutafuta maarifa kwa kujisomea, kusikiliza, video, sauti ambazo zinakupa maarifa ya kujenga familia, jamii na taifa.
Watu wengi hukosa muda wa kujitafuta na kujiuliza “Wewe ni nani?”, “Kwanini uko duniani?”, “Unapaswa kufanya nini?”
Pia wanashindwa kujitafakari na kujitathmini, badala yake wamezidiwa na mbio za maisha, kazi na marafiki hivyo kujikuta wakikimbizana na kazi na kuacha kukimbiza ndoto zao.
Kuwa na mwendo wa kasi katika maisha ni kitu muhimu, lakini kwenda kasi bila kuwa na mwelekeo si kitu chema, weka dira yako ama mwelekeo wako katika namna inavyostahili.
Kadiria mbio zako kisha kimbilia ndoto zako mpaka uzifikie.
Wengine hujikuta wakitafuta furaha maishani mwao na kujikuta wakikimbizana na furaha kwa kudhani kuwa wakipata kitu fulani watakuwa na furaha.
Kwa bahati, wengine hukipata kile wanachokitamani, lakini badala ya kujitosheleza na kupata furaha wanayoitamani, hujikuta hawana hiyo furaha.
Wanatafuta vitu vingi wanavipata au kuvikosa lakini hawapati furaha ya kutosheleza.
Hatujui ya kuwa furaha haitokani na wingi au uchache wa vitu ulivyonavyo, furaha ya kweli ni kuwa na amani ya kweli na kuridhika na vile ulivyonavyo haijalishi ni vingi au vichache.
Tunapaswa kuwa na malengo, kutimiza wajibu katika utendaji kazi utakaotufikisha katika malengo husika na hata tunapofanikiwa – ikiwa tuko katika malengo yetu tuliyojiwekea – ndipo tunapoweza kujitathmini pia na kuona iwapo tumefanikiwa ama kukwama kwa kiwango gani, changamoto zilizopo na namna ya kuzikabili.
Watu wengi hufanya kazi masaa machache huku wakitumia masaa mengi kujipumzisha, kupiga zogo, kujistarehesha, kutembea na marafiki, makundi yasiyofaa, ndiyo maana mafanikio kwao yanabaki kuwa ndoto.
Muda ni mali, tunapaswa kuutumia vizuri sasa maadam tunao, tusiutumie vibaya kwa sababu hauwezi kurejea.
Ndege wanaofanana huruka pamoja. Nakutakia mafanikio katika maisha yako.
Post a Comment